Tuesday, April 19, 2011

Wazanzibari wakijipanga watapiga hatua kubwa ya maendeleo

Na Mwandishi Wetu

"UMOJA ni nguvu, utengano ni udhaifu. Mkataa wengi mchawi. Kidole kimoja hakivunji chawa".

Ni baadhi ya misemo ya Kiswahili yenye maana ya kuhimiza umoja na kuonesha kwamba unasaidia kufikia malengo.


Ni dhahiri kwamba misemo hii imekuja kutokana na ukweli kwamba umoja ni jambo muhimu na lenye manufaa katika jamii.

Mzee mmoja alikuwa na watoto wake watatu na akataka kuwaonesha manufaa ya umoja baina yao. Akachukua fimbo tatu akaziunganisha na kuwataka kila mmoja avunje.

Wote watatu walishindwa kuvunja fimbo zile. Akazifungua na akampa kila mmoja ya kwake na kuwaambia wavunje. Bila kutumia nguvu nyingi kila mmoja akavunja fimbo aliyopewa.

Baba yule akafanikiwa kufikisha ujumbe kwa watoto wake kuwa umoja unasaidia kuwalinda kutoka kwa maadui, tofauti na kila mmoja akiwa peke yake.

Zanzibar kwa maana ya visiwa vya Unguja na Pemba imepitia katika vipindi tofauti na kuna wakati ilikwama kupiga hatua za maana za maendeleo kutokana na kutokuwa na umoja.

Kwa nyakati tofauti kabla na baada ya Mapundizu ya Zanzibar ya mwaka 1964, wananchi wa Unguja na Pemba walitetereka huku wakikumbwa na uhasama mkubwa hasa uliotokana na vyama vya siasa.

Kabla ya Mapinduzi wananchi walijigawa na kujenga tofauti kubwa miongoni mwao kutokana na ushabiki wa vyama vya siasa na hali hiyo iliibuka upya baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Lakini, mambo sasa yamebadilika baada ya kifikiwa kwa maridhiano baina ya vyama vikubwa vya siasa vya Zanzibar, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).

Maridhiano hayo yaliwezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambayo sasa iko madarakani na imerudisha utulivu na upendo kwa wananchi.

Sasa Wazanzibari hawabaguani kwa sababu za kitikadi za kisiasa bali wanashirikiana katika kujiletea maendeleo.

Mazingira haya mazuri ambayo ndiyo kazi kubwa ya serikali yakichanganywa na juhudi za wananchi na sekta binafsi yana nafasi kubwa ya kuifanza Zanzibar kupiga hatua kubwa ya maendeleo tena kwa haraka zaidi.

Waswahili husema 'haba na haba hujaza kibaba' kwa maana kwamba ukiunganisha kidogo kidogo unapata kingi. Vilevile kwa kuunganisha nguvu itakuwa rahisi kwa wananchi kupita maadui wakubwa watatu, ujinga, umasikini na maradhi.

Kwa miaka mingi, Taifa letu limekuwa likipiga vita maadui hao watatu, lakini ni ukweli kwamba vita hiyo inaonekana kushindwa; kwa hiyo juhudi za pamoja badala ya kila mmoja na lake sasa zinahitajika.

Kwa kutambua hilo, gazeti la Majira linalomilikiwa na Kampuni ya Business Times Limited (BTL) limeamua kwa dhati kuhamasiha maendeleo ya wananchi wa Tanzania wakiwemo wa visiwa vya Unguja na Pemba.

Inafaa kujiuliza ni kwanini hatuendelei? Iwapo kweli maendeleo yanahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora, haya mambo kweli hayapo?

Ukweli ni kwamba yapo, lakini kwa utaratibu wa kutafuta maendeleo huku tukiiga mtindo wa maisha ya Warumi katika hatua ambayo utawala wao uliangukia pua, itakuwa vigumu mno kupata mafanikio.

Warumi walitambua kwamba siri kubwa ya kuweza kuwa na nguvu ni kuigeuza michezo hasa ile ya kutumia nguvu kama ndiyo utamaduni wao wa maisha. kwa hiyo kijana wa kirumi akawa anapimwa uwezo wake kwa jinsi anavyoweza kucheza mieleka, kurudiha mikuki, kukimbia na michezo ya namna hiyo.

Lakini, wao hawakuifanya kama ni michezo ya kuinua mizuka bali ni ya kujenga ujasiri na kujenga dhana kwamba mwanamume hafi kitandani bali vitani.

Kwa mwelekeo huo, Warumi wakaitawala dunia, lakini walipofika kwenye kilele cha mafanikio wakajisahau na kuanaza kujiingiza katika anasa. Hali hiyo, iliwafanya wabweteke na wale watwana waliokuwa wakiwatumikia wakawapindua.

Kwa bahati mbaya sasa tunaishi katika mazingira yale yale ambayo yaliwaangusha Warumi huku dhana ikijengwa kuwa maendeleo ni kuwa na uwezo wa kujafaharisha kwa watu.

Dhana hiyo ikibadilishwa na utamaduni endelevu na kuwa na upendo miongoni mwetu na tukaamini kwamba kutokana na nguvu za sasa za kiuchumi na mabadiliko yanayotokea duniani si rahisi kwa mtu mmoja mmoja kuleta maendeleo peke yao.

Lakini, nguvu za mmoja mmoja zikiratibiwa vyema na kuunganishwa zina nafasi kubwa ya kuleta maendeleo kwa walio wengi na kupiga vita kisayansi ujinga, umasikini na maradhi.

Kwa kuelewa hilo, wananchi wa Zanzibar waishio Dar es Salaam wameamua kwa kauli moja kuungana na kwa kushirikiana na wenzao wanaoishi mikoa mingine ya Tanzania na nje ya nchi kusaidia maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Mambo ambayo watayafanya watashiriiana na wananchi wa Unguja na Pemba ili kusaidia kuongeza nguvu ile kasi ya maendeleo iliyopo sasa.

Kwa kutambua umuhimu huyo, Diaspora ya Zanzibar imejipanga kusaidia maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba ili kusaidia juhudi za serikali na wananchi.

Wananchi wa Zanzibar wanaoishi Dar es Salaam wameamua kujitolea kusaidia maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba kwa kuwashirikisha wananchi.

Diaspora ya Zanzibar imekutana mara tatu kujadiliana juu ya suala hilo la kusaidia maendeleo ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Kamati ya Muda ya uongozi wa Diaspora ya Zanzibar katika vikao hivyo imefikia maazimio kadhaa likiwemo la kuwatumia pia watu wa Zanzibar wanaoishi nje ya Tanzania kusaidia maendeleo ya kwao.

Pia kuunda Kamati ya Maendeleo ya Unguja na Pemba ambayo itakuwa na wajumbe kutoka wilaya zote 10 za Zanzibar.

Maazimio mengine ni kuratibu juhudi za wadau ili ziweze kuthaminiwa na walengwa, kuunganisha juhudi za maendeleo na kuanza jambo moja la maendeleo kati ya elimu, tiba, maduka na ufugaji wa kuku wa kienyeji.

Mengine ni kujenga utamaduni endelevu, kufungua akaunti na kusajili umoja ambao ulipendekezwa uitwe Taasisi ya Maendeleo ya Wazanzibari.

Pia Diaspora ya Zanzibar ilikubaliana kutumia Majira kama chombo cha mawasiliano kati ya watu wa Unguja na Pemba na kulitumia kama sekretarieti yao ya kupeleka ujumbe kwa wadau wa Unguja na Pemba na kuratibu juhudi zao za maendeleo.

Ilielezwa kuwa taasisi itakayoundwa itakuwa inaangalia maendeleo ya Wazanzibari tu na kamwe haitajiingiza katika siasa wala udini na ukabila.

Diaspora ya Zanzibar itakutana tena Aprili 14 saa 8 mchana hoteli ya Abla iliyopo Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Dar es Salaam.

Kwa kukuza upendo na kwa kushirikiana kwa pamoja nafasi ipo ya Zanzibar kuwa njema atakaye aje.

No comments:

Post a Comment